Monday, January 6, 2014

"Zitto alianza siku nyingi kuchafua Chadema"....Tundu Lissu

LICHA ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuweka zuio la muda kwa Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujadili uanachama wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Kabwe Zitto, Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Mjumbe wa CC, Tundu Lissu amedhihirisha wazi kuwa chama kimemvua Zitto uanachama.


Lissu ambaye pia ni Wakili wa Chadema katika shauri hilo la zuio, jana katika mkutano na waandishi wa habari na viongozi wa Chadema kuhusu tamko la hatua iliyochukuliwa dhidi ya wanachama watatu waliovuliwa nyadhifa zao akiwemo Zitto, bila kujali zuio alikiri mbele ya waandishi hao kuwa Zitto ataendelea kuwa Mbunge na mwanachama kwasababu ya Mahakama na si matakwa ya chama hicho.
“Ni wazi kuwa harakati zao hasa Zitto za kukichafua chama hazikuanza leo, ni njama zilizoanza muda mrefu sana, hao ni wahusika wa uhaini na usaliti kwa chama na kwa hakika Zitto ataendelea kuwa Mbunge na mwanachama kwa sababu ya Mahakama tu na si kwa matakwa ya Chadema,” alisema Lissu jana katika mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika katika makao makuu ya Chadema, jijini Dar es Salaam.
Kwa kauli hiyo ya Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), ni wazi pamoja na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika kueleza waandishi juzi kuwa CC haikujadili uanachama wa Zitto, kutokana na zuio la Mahakama Kuu, uanachama na uongozi wa Zitto ulijadiliwa hadi kumpa kibali Lissu kutoa kauli hiyo, inayodhihirisha uanachama wa Zitto kwa sasa unashikiliwa na Mahakama tu na Chadema ilishafanya uamuzi.
Kabla ya kauli ya Lissu, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa aliwaeleza waandishi wa habari katika mkutano huo kuwa CC haikujadili wala kuamua kuhusu uanachama wa Zitto kutokana na amri ya Mahakama na kwamba mara baada ya uamuzi wa Mahakama, hatua hiyo itafuata na uamuzi utakaofikiwa kutokana na maazimio ya Kamati Kuu, utatolewa kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
Mbali na Zitto, wengine ambao ni watuhumiwa waliofukuzwa uanachama na CC katika tamko la awali la chama, lililotolewa jana katika mkutano huo na Dk Slaa ni aliyekuwa Mjumbe wa CC, Dk Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.

SHARE HABARI HII KWA RAFIKI ZAKO HAPA CHINI==>>

KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU BASI BOFYA "LIKE" HAPO CHINI KUUNGANA NASI KWENYE FACEBOOK.

0 comments em “"Zitto alianza siku nyingi kuchafua Chadema"....Tundu Lissu”

Post a Comment

 

Mambomseto News Copyright © 2011 -- Template created by O Pregador -- Powered by Blogger

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter